WANANCHI wa kata za Loya na Lutende katika wilaya ya Uyui
mkoani Tabora wametoa kilio chao kwa Waziri wa Mawasiliano,Sayansi na Teknolojia
Prof Makame Mbarawa, wakimwomba
kuwatatulia kero yao ya siku nyingi kwa kuwawekea mnara wa mawasiliano
kwa ajili ya kupata huduma za simu za mkononi.
Kilio hicho wamekitoa mbele ya Mbunge wa Jimbo la Igagula
Dk Athuman Mfutakamba wakati wa ziara yake ya siku nne katika jimbo hilo ya
kukagua utekelezaji wa ilani ya chama cha Mapinduzi pamoja na miradi mbali
mbali ya maendeleo ya wananchi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Wananchi hao wamesema kata
hizo ni miongoni mwa kata ambazo hazina mawasiliano ya aina yeyote ile katika
jimbo la Igalula kutokana na kutokuwa na mnara hata mmoja wa kuwasaidia kufanya
mawasiliano hivyo kuwafanya wananchi hao kuwa nyuma kimaendeleo.
Wamebainisha kuwa kilio hicho cha kuomba kuwekewa minara
kimekuwa ni cha siku nyingi na hakijapatiwa ufumbuzi zaidi ya kupewa
ahadi hewa mbunge wao kila mara, hali
inayowafanya baadhi yao kuichukia serikali ya chama cha mapinduzi kwa kuona
kuwa haiwajali wananchi wake lakini kumbe wapi jamani.
Diwani wa kata ya Lutende Bwana Pancras Luge amesema Kilio
cha wananchi wake ni mnara wa mawasiliano, na kwamba hapa hawawezi kuongea na
simu hata kama kuna tukio la mauaji kama si kukanyaga baiskeli kwenda kutoa
taarifa sehemu husika.
Luge amesema hivi sasa hawezi kupita barabarani kifua mbele
kwani amekuwa akitukanuwa sana na wananchi kutokana na kukosekana kwa
mawasiliano hayo ya Simu.
Akijibu tuhuma za wananchi dhidi yake Mbunge wa Jimbo hilo Dk Athuman Mfutakamba
amesema Serikali tayari imeshatenga fedha kwa ajili ya minara hiyo na
mkandarasi tayari yupo na kuongeza kuwa yeye kama mbunge wao atafanya mawasiliano
na Waziri anayehusika ili kuhakikisha wananchi wa Loya na Lutende wanapata
mawasiliano ya simu za mkononi.
Nikiripoti kutoka wilaya ya Uyui mimi ni dikodiko.nyagale
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
mwanga wetu maoni