Mbunge wa Nzega, Dk Khamis Kigwangalla, (CCM), leo anatarajiwa kuanza kukusanya saini za wabunge akitafuta kuungwa mkono katika hoja ya kutokuwa na imani na Spika wa Bunge, Anne Makinda kwa madai kwamba amekuwa akikiuka kanuni za Bunge.
Dk Kigwangalla aliibua hoja ya
kutokuwa na imani na Spika katika kikao cha wabunge wote cha kuelezea
shughuli zitakazofanywa na Bunge katika mkutano wa 13, kilichofanyika
juzi jioni kwenye ukumbi wa Pius Msekwa.
Mbunge huyo ambaye pia ni Mwenyekiti
wa Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, jana
alithibitisha kuwapo kwa mjadala huo katika kikao cha wabunge, lakini
hakuwa tayari kueleza kwa undani na badala yake alisema kwamba leo
ataanza kukusanya saini za wabunge kwa ajili ya kukamilisha hoja ya
kutokuwa na imani na Spika Makinda.
Chanzo chetu kutoka katika kikao
hicho cha wabunge kilibainisha kuwa Kigwangalla alihoji kuhusiana na
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Andrew Chenge (CCM-Bariadi
Magharibi) kuteuliwa na Spika wakati katika kamati nyingine wenyeviti na
makamu huchaguliwa na wajumbe wa kamati husika.
Pia Dk Kigwangala alisema Spika
Makinda alivunja kanuni kwa kuwapa posho ya Sh430,000 kwa siku wajumbe
wa kamati inayoongozwa na Chenge wakati wajumbe wa kamati nyingine
wamekuwa wakipewa Sh130,000.
“Anachokifanya Spika ni matumizi
mabaya ya fedha za umma, inakuwaje wengine wafanye kazi hata bila posho
lakini wao (Kamati ya Bajeti), walipwe posho ya Sh430,000 kwa siku?”
chanzo hicho kilimkariri Dk Kigwangalla akihoji. Hata hivyo, Katibu wa
Bunge, Dk Thomas Kashililah akizungumza na gazeti hili jana alisema
mazingira ya kamati fulani kupata malipo ya ziada tofauti na viwango vya
kawaida hutokea pale uongozi wa kamati husika unapoomba kwa Spika.
“Si kweli kwamba Kamati ya Bajeti
inalipwa fedha za ziada kila wakati, hapana, ni pale tu wanapoomba
malipo hayo kutokana na sababu ambazo lazima Spika aridhike nazo.
Ieleweke kuwa siyo kamati hiyo tu, kwa sasa Kamati ya Katiba, Sheria na
Utawala ambayo inachambua miswada mingi nayo imekuwa ikiomba na baada ya
Spika kuridhia basi nao wanapewa,” alisema Dk Kashililah.
Katibu huyo wa Bunge alieleza kuwa
zaidi ya kamati nane zimewahi kuomba malipo ya ziada kwa maana ya kutaka
posho zaidi, ulinzi, usafiri na hata chakula, ikiwa zinakabiliwa na
majukumu ya ziada pia katika mazingira tofauti nje ya utaratibu wa
kawaida.
“Kimsingi, kamati nyingi zinapewa
malipo tofauti, watu wanaweza kuwa na kazi mpaka saa saba au nane usiku,
au wanakwenda kufanya kazi katika mazingira yasiyokuwa ya kawaida,
taratibu zinamruhusu Spika kama akiridhika na maelezo ya kazi husika,
basi anaruhusu kutekelezwa kwa maombi hayo,” alisema Dk Kashililah.
Kuhusu Serukamba
Aidha, Dk Kigwangalla alinukuliwa
akisema Spika amekiuka kanuni kwa kumchagua Mwenyekiti wa Kamati ya
Miundombinu, Peter Serukamba (Kigoma Mjini-CCM), kuwa mjumbe wa Kamati
ya Bunge ya Bajeti.
“Hakuna mbunge yeyote aliyepo katika
kamati mbili lakini hata kungekuwa na sababu maalumu basi wa kuteuliwa
angekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara,
Mahmoud Mgimwa (Mufindi Kaskazini-CCM) ambaye TRA (Mamlaka ya Mapato
Nchini) ipo chini ya kamati yake,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho kilisema Dk Kigwangalla
alisema badala ya kumweka karibu katika ushiriki, Mgimwa alipokwenda
katika kamati hiyo aliambulia kufukuzwa.
Akizungumzia suala hilo, Dk
Kashililah alisema Serukamba pamoja na wabunge wengine kadhaa
waliteuliwa na Spika kwa ajili ya kuongeza nguvu katika kamati hiyo
wakati wa kipindi cha Bajeti Kuu ya Serikali.
Aliwataja wabunge wengine
walioteuliwa kushiriki katika Kamati ya Bunge ya Bajeti kuwa ni John
Cheyo (Bariadi Mashariki-UDP), Salahe Pamba (Pangani - CCM) na Hamadi
Rashid Mohamed (Wawi - CUF).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
mwanga wetu maoni