(Dikodiko nyagale)
Kutokana
na hatua ya Samson Mwigamba, aliyesimamishwa uenyekiti wa CHADEMA Mkoa
wa Arusha, kukiri mbele ya waandishi wa habari kuwa amevunja katiba,
kanuni, maadili, miongozo, taratibu na itifaki za chama kwamba yeye
ndiye aliyeandika (kwa kutumia jina bandia);
Kwenye
mitandao ya kijamii, waraka uliojaa uongo, upotoshaji na uchonganishi
kwa wanachama na viongozi, Idara ya Habari ya CHADEMA (kupitia Ofisa
Habari, ambaye alikuwepo kwenye kikao hicho) imechukua hatua ya kuanza
kutoa na kuandaa utolewaji wa taarifa rasmi zinazojibu uongo, upotoshaji
na uchonganishi ulioandikwa na Mwigamba, ili kuweka kumbumbu sawa,
wanachama na Watanzania wote waelewe.
Kwa kuanzia, leo tunatoa ufafanuzi juu ya suala la kikatiba la ukomo wa uongozi ndani ya chama.
Kupitia
taarifa hii ya Idara ya Habari, kwanza tunapenda kushangazwa na hatua
ya Mwigamba kuendelea kuvunja katiba, kanuni, maadili, miongozo,
taratibu na itifaki ya chama, ambapo kupitia vyombo vya habari
ameendelea kutunga mambo yasiyokuwepo badala ya kuwasilisha hoja zake
(kama anazo) kupitia vikao halali vya chama ambavyo yeye anao uwezo wa
kuitisha au kuhudhuria.
Tungependa
umma ufahamu masuala kadhaa, kwamba katika kikao cha Baraza la Uongozi
wa Kanda ya Kaskazini (Tanga, Manyara, Kilimnajaro a Arusha), muda mfupi
kabla Mwigamba hajatuhumiwa kwa usaliti na hujuma, alikuwa ametoka
kuwasilisha taarifa ya hali ya chama katika mkoa wa Arusha.
Kupitia
taarifa yake hiyo Mwigamba alisifia viongozi wa chama taifa kwa
kusimamia maslahi na matakwa ya Watanzania katika hoja au agenda
mbalimbali pamoja na kuendesha chama vizuri. Akamsifia Mbunge wa Arusha
Mjini, kwa juhudi zake za uenezi na uimarishaji wa chama.
Aidha
baada ya kubainika kwa tuhuma hizo, pamoja na uthibitisho uliokuwa
chini ya waraka huo, uliotumika na wataalam wa kompyuta kubainisha pasi
na shaka kuwa waraka ule umetoka na umehifadhiwa kwenye kompyuta yake,
Mwigamba alipoulizwa alikana kabisa mbele ya kikao, akisema hahusiki
wala haijui ‘article’ ile ilitokea wapi, hadi alipolazimika kuandika
maelezo yake chini ya kiapo.
Jana mbele ya waandishi wa habari ameendelea ‘kugeuka-geuka’, akizungumza lugha tofauti tofauti kwenye suala moja.
Pili,
kupitia taarifa hii kwa umma, Idara ya Habari ya CHADEMA, inaweka hapa
chini kumbukumbu sahihi juu ya kauli ya upotoshaji, uongo na
uchonganishi ya Mwigamba kuwa uongozi wa juu wa chama ‘umechakachua’
katiba kwa kuondoa kipengele cha ukomo wa kushika madaraka ya uongozi
ndani ya chama.
Kumbukumbu
hii sahihi inatokana na ufafanuzi uliotolewa katika mitandao ya kijamii
(baada ya kuombwa na watu wengi) na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi,
John Mnyika, ambaye alikuwa Katibu wa Kamati iliyohusika na uandikaji
upya wa Katiba ya CHADEMA ya mwaka 2006, ambayo ndiyo inatumika hadi
sasa.
Ufafanuzi
wenyewe ni huu (una sehemu mbili, kwa nafasi yake, pia maoni yake
binafsi). Madai ya kwamba “Wakati tukifanya mabadiliko ya katiba mwaka
2006 hatukugusa kipengele kinachomzuia kiongozi kuongoza kwenye nafasi
moja kwa zaidi ya vipindi viwili vya miaka mitanomitano. Lakini wakati
katiba inachapwa chini ya uongozi uliopo, kipengele hicho kiliondolewa
kinyemela”; hayana ukweli kwa kadiri ya ufahamu wangu.
Mosi,
mwaka 2006 hatukufanya marekebisho ya katiba bali tuliandika upya
katiba ya chama kutoka ile ya mwaka 2004. Waraka uliandikwa nchi nzima
kwa wanachama kutoa maoni na kuwasilisha makao makuu kuanzia kwenye
ngazi zao za chini za kikatiba.
Baada
ya kukusanya maoni kulikuwa na timu tatu, timu moja ilihusu kuandika
falsafa na itikadi ya chama ambayo Mwenyekiti wake alikuwa Profesa
Baregu na katibu wake nilikuwa mimi.
Sehemu
hiyo ya katiba niliandika neno kwa neno mapendekezo ya awali kwa
kuzingatia mapendekezo yaliyotolewa, tulifanya mapitio pamoja na Profesa
Baregu na hatimaye ikaingia kwenye vikao vya kikatiba vya chama na
kupitishwa.
Sehemu
ya falsafa kwa sehemu kubwa tulinukuu kwenye katiba kama ilivyokuwa
mwaka 2004, sehemu ya itikadi tuliandika upya kabisa haikuwepo katika
katiba ya CHADEMA ya zamani.
Sehemu
zingine katika katiba kwa sehemu kubwa kazi ya kuunganisha maoni mapya
na kufanya pia rejea kwenye katiba ya zamani ilifanywa na timu ya watu
watatu tukiongozwa na muasisi wa chama Mzee Victor Kimesera pamoja na
Mkurugenzi Benson Kigaila na mimi.
Kulikuwa
na timu nyingine ya kuandaa miongozo ya mabaraza ya chama: Baraza la
Wazee, BAVICHA na BAWACHA ambao nao walifanya kazi kwa upande wao na
nilishiriki katika kupendekeza mwelekeo na mapitio ya kulinganisha
rasimu ya miongozo yao na rasimu ya katiba ya chama.
Kwa
ninavyokumbuka hicho kinachoitwa “kipengele kinachomzuia kiongozi
kuongoza kwenye nafasi moja kwa zaidi ya vipindi viwili vya miaka mitano
mitano” hakijawahi kuingizwa kwenye katiba mpya ya CHADEMA.
Baada
ya timu zote kufanya kazi yake; rasimu ya katiba ilipita katika vikao
vyote vya kikatiba yaani sekretariati, kamati kuu, baraza kuu na
hatimaye mkutano mkuu. Katika vikao vyote hivyo, iwapo kipengele hicho
kingekuwa kimeondolewa ‘kinyemela’ kama inavyodaiwa, mwandishi wa tuhuma
hiyo angehoji toka Agosti 2006.
Aidha,
baada ya katiba kupitishwa na kuanza kutumika kifungu hicho kingekuwa
kimeondolewa kinyemela kati ya mwaka 2006 mpaka 2008 mtoa madai au mtu
mwingine yeyote ndani ya chama angekuwa amehoji wakati wa matumizi.
Kumekuwepo pia mchakato wa kufanya marejeo kwa ajili ya kushughulikia
makosa ya uchapaji (errata) kwa nyakati mbalimbali, suala hili si kati
ya mambo yaliyoibuliwa.
Mwaka
2009 CHADEMA kilifanya uchaguzi mkuu wakae mkuu nchi nzima ambapo
vifungu vya masuala ya uchaguzi wa ndani ya chama vilifanyiwa rejea mara
kwa mara. Mwandishi wa madai hayo alikuwepo wakati huo, suala hili la
kwamba kuna kifungu kimeondolewa kinyemela sikulisikia likilalamikiwa
kwenye vikao vyovyote vya kikatiba iwe ni sekretariati, kamati kuu,
baraza kuu na mkutano mkuu.
Kwa
vyovyote vile kwa historia ya chama toka mwaka kilipoanzishwa mpaka
wakati huo wa uchaguzi wapo viongozi ambao walikuwa wanagombea wakiwa na
vipindi viwili wakati huo kwenye cheo kimoja cha ngazi moja; kifungu
hicho kingekuwepo toka 2006 kingetumika kuwawekea mapingamizi. Na kama
kingekuwa ‘kimeondolewa kinyemela’ kungekuwa na malalamiko mengi kiko
wapi kwa kuzingatia ‘joto’ la uchaguzi wa wakati huo.
2010
mpaka 2013 madai hayo hayajawahi kutolewa kwenye kikao chochote cha
kikatiba katika ngazi ya taifa kwa kuwa mimi ni mjumbe wa vikao vyote
vya kitaifa ambavyo yeye amesema kwamba ni mjumbe.
Madai
kama hayo yangetolewa na asiye mwanachama au walau mwanachama wa
kawaida tungesema tu ni maoni ya kawaida yaheshimiwe na aelimishwe.
Lakini madai kama hayo yakitolewa na kiongozi wa chama mwenye nafasi ya
kuujua ukweli wote huo yanaacha maswali kuhusu dhamira yake. Naamini
mamlaka zinazohusika za chama zitatumika katiba, kanuni, maadili na
itifaki kuchunguza na kuchukua hatua kuanzia kwenye ngazi yao huko tukio
lilipotokea.
Maoni binafsi ya John Mnyika katika suala hili
Hata
hivyo, kwa maoni binafsi (yasichukuliwe kuwa ni kauli ya nafasi
ninazoshikilia kwenye chama), dhamira ya haya inajionyesha kwenye andiko
lenyewe la muhusika kuanzia aya ya kwaza “ Kufuatia malumbano
yanayoendelea kwenye vyombo vya habari namadhaifu mengi ambayo
tumeshayashuhudia kwenye chama kwa sasa, natoa wito kwawana CHADEMA wote
nchini kwamba wakati umefika tubadilishe uongozi wa juu wachama.
Mtoa
madai anaendelea kuandika kwamba “ Ni muhimu wanachadema mkafahamu
kwamba kitendo cha kuondolewa kwa kipengele hicho ndicho kinacholeta
mpasuko leo kwenye chama unaotokana na Mbowe na Zitto kupigania
uenyekiti. Kama kingekuwepoleo Mbowe alikuwa anakatazwa na katiba
kugombea kipindi cha tatu na hivyo vita iliyopo kati yake na Zitto
isingekuwepo na chama kingekuwa imara zaidi. Ni dhahiri Mbowe aliondoa
kipengele hicho kwa makusudi ili aweze kuendelea kugombea bila mwisho na
huu ni udikteta kama ule tu wa akina Lyatonga Mrema, John Cheyo na
wengineo, na wanachadema hatupaswi kuuruhusu si kwa Mbowe tu balikwa
yeyote atakayepata nafasi ya kuwa mwenyekiti wa chama chetu.
Anaendelea
kuandika madai mengine mengi ya upotoshaji lakini mwishoni anamalizia
kwa dhamira yake ile ile “Nitaendelea kuwadondolea ili muonekwa nini
napendekeza tuung'oe uongozi huu chini ya Mbowe.”. Kwa hiyo, dhamira
yake ni uchaguzi na mabadiliko ya uongozi; dhamira yeyote njema ifuate
mkondo wa katiba, kanuni, maadili na itifaki; kinyume chake ni ‘njama
ovu’ na ‘utovu wa maadili”.
Nimekuwepo
chaguzi mbili kuu za CHADEMA 2004 (nikiwa mtazamaji sio mwanachama) na
2009 nikiwa katikati ya chaguzi hizo kama kiongozi. Naamini uchaguzi huu
wa chama ulioanza kuanzia mwaka huu 2013 utakamilika mwaka 2014 CHADEMA
ikiendelea kusimamia dhima yake ya kuleta uongozi bora, sera sahihi,
mikakati makini na oganizesheni thabiti kwa maendeleo endelevu ya nchi
yetu.
JJ
Imetolewa leo Jumanne, Oktoba 29, 2013 na;
Tumaini Makene
Ofisa Mwandamizi wa Habari-CHADEMA
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
mwanga wetu maoni